SABATO
Kutoka 20:8 “Ikumbuke siku ya sabato uitakase”..
Sabato ni neno la kiyunani linalotokana na aneno “shabbath” linalomaanisha pumziko (rest). Neno hili kwa kingereza huitwa Sabbath” linalomaanisha pia maana ile ile pumziko.
Katika juma la uumbaji (mwanzo sura ya 1) Mungu anafanya kazi zake kwa siku siku akiumba vitu vyote vilivyo duniani. Katika siku ya saba yeye mwenyewe (Mungu) anapumzika na kustarehe. Mwanzo 2:1-4 Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya. Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa. Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi. Chimbuko la pumziko letu ni Mungu mwenyewe.
Wana wa Israeli katika safari ya kutoka Misri kwenda Kaanan Mungu anawakumbusha juu ya upendo wake kwao. Na hivyo anawapa taratibu ya namna ambavyo sasa imewapasa kuenenda kwa kicho mbele za Mungu. Katika mlima Sinai Mungu anampa Musa mbao mbili za mawe zikiwa na amri 10. Ambazo zilikuwa katika mgawanyiko wa Amri 4 kwa Amri 6. Zenye amri 4 zilihimiza juu ya upendo wa Mwanadamu kwa Mungu, zenye amri 6 zilihamasisha juu ya upendo wa mwanadamu kwa mwanadamu mwenzake. Ndio maana Yesu anawaambia wanafunzi wake juu ya amri anaelezea kwa ufupi “amri kuu ndio hii umpende Bwana Mungu wako………, nay a pili nayo yafanana nayo mpende jirani yako kama nafsi yako” Mthayo 22:37-40.
Katika amri hizi 10, amri ya 4 huzungumza kwa upana juu ya sabato. Kutoka 20:8 Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Swali la kujiuliza. Kwanini Mungu anawaambia waikumbuke??? Kukumbuka jambo Fulani maana yake ni kwamba huenda ulisahau, na hata hivyo huwezi ukakumbuka kitu ambacho hakikuwahi kuwepo. Bila shaka habari ya sabato ilikuwepo hata kabla ya wana wa Israeli kwenda utumwani Misri. Lakini kwanini Mungu anawataka waikumbuke sabato je waliisahau kweli? Kumbuka kuwa taifa la Misri halikumtambua Mungu na ndiyo maana Musa alipomuendea Farao kuomba ukubali ili wana wa Israeli waondoke alimuuliza Musa Mungu wenu ni nani? Mwanzo 5:2…. Maana yake ni kwamba wamisri waliabudu miungu Kutoka 12:12 Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. Kwahiyo wana wa Israeli hawakupata muda wa kumuabudu Mungu wao kwakuwa walitumikishwa.
Mungu anawataka wana wa Israeli waikumbuke sabato na kuitakasa (kutakasa maana yake kuifanya kuwa safi) wasiihalifu, wasiinajisi, wasiidharau (isaya 58:13). Waifanye kuwa siku maalum kama yeye alivyofanya siku ya saba kuwa maalum kwa kupumzika kuitakasa na kuibariki. Mungu anawaamuru wanaisraeli kuzitakasa sabato zake kwakuwa ni ishara kati ya Mungu na wanadamu. Ezekiel 20:12,20 Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye…… zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. “Sabato ni ishara kati ya Mungu na wanadamu”
JE SABATO ILIKUWA NI KWA AGANO LA KALE PEKEE??
Kumekuwepo na dhana mbali mbali kuwa sabato ilikuwa tu ni kwa ajili ya wayahudi peke yao je Yesu mwenyewe alipokuwa duniani aliitunza sabato?
Luka 4:16 Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Marko 6:2 Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake……. Yesu pia alikuwa na kawaida ya kuingia katika sinagogi na kusali siku ya sabato
Je huenda Yesu mwenyewe kwa kifo chake aliibatilisha sabato kwa kuwa twaelewa kuwa sheria za wana wa Israeli nyingi zilikuwa ni kivuli cha msalaba. Mathayo 5:17 Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Yesu anatangulia kutupa angalizo kuwa yeye hakuja kuitangua torati (sheria) bali kuitimiliza (kuitiisha). Ieleweke kuwa katika mambo yaliyokuwa yakiishia msalabani kwa kifo cha Yesu amri 10 za MUNGU hazimo. Hizi bado ziliendelea kuwepo na bado zipo na zitakuwepo kwakuwa ni agano la milele. Na ni hizi amri ndizo Yesu anatuambia mwenyewe kuwa hakuja kuziondoa bali kutufundisha ushikaji wake. na hivyo amri ya sabato bado iko palepale kama ambavyo amri zingine pia zipo.
Kama Yesu mwenyewe aliitunza sabato na anatuambia mwenyewe kuwa hakuibadilisha sheria je huenda ni mitume ndio waliobadilisha amri ya sabato? Matendo 16:13 Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mtume paulo na sila wakiwa makedonia waliitunza sabato na walikutana siku ya sabato kusali. Matendo ya mitume 17:2 Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu,………… matendo ya mitume 18:4 Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani.. Hata mitume pia waliitunza sabato na Paulo pia alikuwa na desturi ya kutoa mafundisho katika sinagogi kila sabato.
JE SABATO ITAISHIA TU HAPA DUNIANI?
Isaya 66:22, 23Kama vile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazofanya, zitakavyokaa mbele zangu, asema Bwana, ndivyo uzao wenu na jina lenu litakavyokaa. Na itakuwa, mwezi mpya hata mwezi mpya, na sabato hata sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema Bwana. hii hutuambia dhahiri kuwa sabato haitaishia tu kutunzwa hapa duniani lakini hata mbinguni watakatifu wa Bwana watajihudhurisha mbele za Bwana panapo sabato naam hata katika nchi tutamwabudu Mungu wetu. kadiri mbingu na nchi zitakavyodumu, sabato itaendelea kuwa ni alama ya uwezo wa Muumbaji
JE SIKU YA SABATO NI LINI HASA? (IJUMAA, JUMAMOSI AU JUMAPILI?)
Kumekuwa na madai mengi sana kuwa sabato iliishia msalabani kitu amabacho si kweli, wengine wanadai biblia haijaweka wazi kuwa ni ipi hasa kweli siku ya sabato kwahiyo ni radhi kusali siku yoyote hata jumanne jumapili ijumaa nk…. Lakini je Biblia inatuambia nini kuhusu siku halisi ya sabato??
Mungu aliumba mbingu na nchi kwa siku 6 na siku ya saba akapumzika maana ilikuwa ni sabato. Mwanzo 2:2 Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Hii hutuonesha moja kwa moja kuwa siku ya sabato ilikuwa ni siku ya saba. Sasa je siku ya saba hasa ni lini? Kwa kawaida leo hii tunahesabu siku kwa majina ya kiarabu (jumampili, jumatatu, jumanne, jumatano, alhamis, ijumaa na jumamosi) na hii ndio hasa huleta shida kwa wengine hasa kwa kuwa neon mosi humaanisha moja basi wao huchukulia jumamosi kama siku ya kwanza na ijumaa kama siku ya saba. Wengine wao huadhimisha jumapili kama siku ya saba (sabato) kwa kuwa ndio siku ya ufufuo kwahiyo kwao sabato siyo siku ya saba bali ni siku ya ufufuo, lakini wengine pia huadhimisha jumamosi kama siku ya sabato kwa kuwa ndiyo siku ya saba.
Hebu tuangalie ushahidi katika biblia.
Luka 23:54 Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia. katika sura nzima ya 23 cha kitabu cha luka na vitabu vingine vya injili kama vile marko 15, mathayo 27 na yohana 19 habari ya kifo cha mkombozi wetu zinaelezwa hapo. Biblia takatifu inatuambia kuwa Yesu alipokamatwa kwa kusudi la kuuawa ilikuwa ni siku ya maandalio ya sabato. Maana yake ni kwamba ailikuwa siku moja kuelekea sabato. Kwa lugha nyingine tutakubaliana kuwa ilikuwa ni siku ya sita nayo siku iliyofuata ilikuwa ni siku ya saba yaani sabato.
Tuangalie pia siku ya ufufuo wake ilikuwa ni lini.
Luka 24:1 Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari. soma pia mathayo28:1, Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. soma marko 16:1 na yohana 20:1. Maandiko yote yako wazi kutuonesha kuwa Yesu alifufuka siku ya kwanza ya juma na pia yanasisitiza kuwa ilikuwa ni baada ya sabato… bila shaka yoyote kama tunaikubali biblia tutakubali kuwa ni kweli Yesu Kristo alikufa siku ya sita (maandalio ya sabato) na akafufuka siku ya kwanza (baada ya sabato)
Maadhimisho ya pasaka leo hii pia yaweza kutupatia mwanga kidogo juu ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo. Dunia nzima inatambua kuwa Yesu alikufa siku ya ijumaa na kafufuka jumapili. Na kama tukishaelewa kuwa Yesu alikufa ijumaa ambayo ndiyo biblia hutuambia kuwa ilikuwa ni siku ya maandalio ya sabato au siku ya sita ya juma je siku inayofuata ni ipi?? Bila shaka ni JUMAMOSI
Vilevile biblia huweka wazi kuwa Yesu alifufuka siku ya kwanza ya juma ambayo bila shaka ni jumapili nayo yatjwa kama siku baada ya sabato je siku inayotanguliwa na jumapili ni ipi? Hakuna hofu kuwa ni JUMAMOSI.
Hii hutupatia hitimisho kuwa Yesu alikufa ijumaa iliyokuwa maandalio ya sabato (Jumamosi) na akafufuka jumapili ambayo ilikuwa ni baada ya sabato. Hivyo tunakubaliana kuwa siku ya sabato ambayo BWANA MUNGU alipumzika, ambayo YESU KRISTO aliingia katika sinagogi na ambayo mitume pia walikutana kusali ilikuwa ni JUMAMOSI.
BWANA AKUBARIKI
BY; PETER JEFTER
0785167164
peterjefter91@gmail.com