Monday, 22 May 2017

TUTAWAONA TENA WAPENDWA WETU


                                TUTAWAONA TENA WAPENDWA WETU TULIOTENGANA NAO
                                                             (WALIOLALA)

1Thesalonike 4:16 Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.

Hakika kuishi pamoja kunaleta furaha maishani. Kusudi la Mungu tangu kuimba dunia ilikuwa ni watu waishi pamoja tena kwa furaha daima wakimtukuza yeye (MUNGU). Lakini ni ale tu adui alipoingilia kati mpango huu mzuri na kuleta yaliyo kinyume. Dunia ikalaaniwa Mungu akatamka maneno makali na machungu kwa mwanadamu ikiwa tu ni matokeo ya kuiasi agizo lake la kutolila tunda mwanzo 2:17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika. Lakini ni pale tu Adam na Hawa walipodanganywa na shetani nao wakalila lile tunda tamko hili lilitimia.

Kwa mara ya kwanza ulimwengu unashuhudia huzuni unaoletwa na matokeo ya dhambi. mwanzo 4:8 Kaini akamwambia Habili nduguye, Twende uwandaniIkawa walipokuwapo uwandani,Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua. Wazazi wetu wa kwanza kabisa wanashuhudia kile Mungu alichowaambia kikitokea katika familia yao. na hivyo kumekuwa na misururu ya matukio ya vifo ambavyo kiuhalisia haviwezi kuelezeka katika lugha ya kueleweka. Matukio kama vile kujiua, kuuawa, ajali za moto majini nchi kavu, magonjwa njaa, majanga ya asili, vita na mengine mengi yamekuwa ni vyanzo vya vifo kwa wanadamu. Lakini ukweli ni kwamba kifo ni MPANGO WA SHETANI.

Ulimwengu wa leo kila kona ni vilio. Kifo ni kibaya, kifo hakitamaniki, kifo hakielezeki wapendwa, kifo hakizoeleki. Jamii inapoteza watu mashuhuri kwa sababu ya kifo, tunawapoteza wapendwa wetu kwa sababu ya kifo, tunapoteza watu tunaowategemea kwa sababu ya kifo, tunapoteza watoto, tunapoteza wenzi, tunapoteza wazazi, tunapoteza marafiki kwa sababu tu ya kifo. Hakika kifo ni mbaya. na kibaya zaidi ni kwamba tunapotengana nao hatuwaoni tena, wala hatuwasikii tena. Wanatuacha na huzuni, kilio, majonzi, shida, dhiki, taabu na mateso mengi, zaidi sana hutupelekea katika misongo ya mawazo na hata kutusabibishia sisi nasi kufa. Habari mbaya ni kwamba hata sisi tulio hai leo ni marehemu watarajiwa

Ni kwa sababu ya kifo hata leo jamii imetofautiana juu ya kile hasa wanachoamini kuhusu kifo. Wengi hudai kuwa mtu akifa ndio mwisho wake wa kuwepo duniani milele na milele (no life after death), dhana hii hudai kuwa mtu akifa anapelekwa pagatori huko ndiko anapokea hukumu yake kutoka kwa Mungu, kama alikuwa mdhambi basi hupokea mateso hukohuko na kama alkuwa mwenye haki basi roho yake huenda peponi kupumzika. Iko dhana nyingine inayoamini katika maisha baada ya kifo (there is life after death). Dhana hii hudai kuwa mtu anapokufa huyarudia mavumbi na husubiri siku ya kiama Bwana atakapokuja kuwachukua watakatifu wake nao waliokufa katika Bwana watafufuka kwanza.

Lakini ukweli hasa kuhusu habari ya wafu iko vipi katika Biblia??

Mwanzo 3:19 kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi. Bwana Mungu alipozungumza na Adam baada ya kula tunda alimwambia atayarudia mavumbi maana ndiko alikotoka. Ama hakika mtu anapokufa huyarudia mavumbi lakini naye hajui lolote muhubiri 9:5 kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. (soma pia Ayubu 14:21). Ni wazi kuwa mtu anapokufa huenda kaburini na hana mawasiliano tena kwa kuwa fahamu zake zimemtoka naye hufanana kama gogo lilikatwa likaangushwa huku likioza.

Habari njema ni kwamaba Bwana wetu Yesu Kristo aliushinda mauti naye ndiye anatupatia ahadi ya kuishinda mauti vilevile. Warumi 5:17 Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo. Yeye Mungu mwenyewe aliyetamka kuwa tutakufa hakika ndiye pekee aliyeishinda mauti na kwa kupitia yeye nasi tutaishinda mauti. (1wakorintho 15:12-28)

Sasa basi ikiwa tutaamini kuwa hakuna maisha baada ya kifo tutakuwa upande wa wale wanaosema hakuna ufufuo nao siku ya kiama (kwa kuwa kama mtu akifa anapokea stahili yake pagatori na roho yake huenda peponi basi hakuna tena ufufuo) nao wanapingana na ukweli juu ya kufufuka kwake Kristo. 1 wakorintho 15:13,14 Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure.

Tunaambiwa ikiwa alifufuka basi nao wafu watafufuliwa……….. lakini kama tutaamini kuwa kuna maisha baada ya kifo tutaamini kuwa kuna ufufuo wa wafu nasi twaamini kuwa Kristo alifufuka katika wafu limbuko lao waliolala. 1wakorintho 15:20 Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Hii ni dhahiri kwamba fundisho juu ya kutokuwepo kwa ufufuo au kusema kuwa wafu huenda pagatori ni kinyume na biblia nayo hupingana na ukweli kuwa Kristo alifufuka.

1 wathesalonike 4:13-18 Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo.

Mtume Paulo hakuacha kuzungumzia habari hii ya wafu kwakuwa mafundisho ya uongo kuhusu hali wafu yamekuwepo tangu zamani. Pualo anawaambia wathesalonike kupitia barua yake kuwa kwa habari ya wafu hakuna haja ya kusiskitika na kuishi bila tumaini kwa kuwa waliokufa katika Bwana watafufuliwa kwanza siku ya marejeo ya pili ya Kristo kuwachukua watakatifu wake. wapendwa ukweli ni kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu na akafufuka ishara ya ushindi. Akatuachia tumaini la kufufuka siku ya mwisho. Swali kwangu na kwako je tunatumaini katika Kristo?? Je tunajiaandaje ikiwa tutakabiliwa na kifo leo tutakuwa tumeweka wapi tumaini letu?

Katika marejeo ya pili ya Kristo atawachukua walio watakatifu wake. kristo atakaporejea atakuta makundi manne ya watu. 1. Kundi la wenye haki walio hai, 2. Kundi la waovu walio hai, 3. kundi la wenye haki waliolala, 4. kundi la waovu waliolala. Angalizo” atakapotokea Kristo mawinguni na jeshi lake la malaika wakizipiga tarumbeta ‘wale wenye haki waliolala watafufuliwa kwanza, wao pamoja na wenye haki walio hai watavikwa miili ya kutokufa na kuondolewa miili ya kufa’. 1 wakorintho 15:52,53 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa. hapo ndipo tutakapoungana kumlaki mwokozi hewani (1 wathesalonike 4:17). Wakati huo, wale waovu waliolala hawatafufuka (isipokuwa wale waliomchoma “ufunuo 1:7’ watakaofufuliwa kushuhudia utimilizo wa kile Kristo alichosema kisha walale tena) nao waovu walio hai watakufa wasioune utukufu wa Mungu kwa sababu ya dhambi zao wakikimbia na kuuambia milima iwasitiri (Ufunuo 6:16). Nao watadumu katika hali ya wafu kwa miaka 1000 huku watakatifu nao wakitawala na Bwana juu mbinguni kwa miaka 1000. Ufunuo 20:4

Wapendwa wangu, kifo si kitu kizuri, kifo hutuletea huzuni nyingi na vilio vikuu kila siku katika maisha yetu. Kifo hututenganisha na wapendwa wetu. Kifo hakibishi hodi, wala hakitoi taarifa. Leo uko hai, kesho unalala, leo tunasalimiana kesho hatusemeshani tena, kifo huja kwa wakati usiotegemewa. Hakuna hata mmoja aliyewahi kujua saa ya kufa kwake. Habari mbaya zaidi ni kwamba kifo hutuijia katika saa tusiyotarajia. Hutuijia katika saa tusiyojiweka tayari. hutuijia katika saa tusipokamilisha mipango yetu. Wengine hukutwa katika nyakati za furaha kabisa kifo huwachukua, wengine wakiwa na malengo makubwa kabisa kifo huwakatisha. Hakika tunateswa sana na kifo. Na tutakufa ni kweli.

Umejiandaaje kabla ya kufa?? Umejiweka tayari kiasi gani wakati huu ungali hai? Tumaini lako umeliweka wapi nyakati hizi una nafasi?? Nakupa shauri, WEKA TUMAINI LAKO KWA KRISTO. Fanya uhusiano mzuri na Kristo madam muda ni sasa. Utakapolala ulale katika tumaini la kumuona Bwana. Maana aliushinda mauti nasi tutaushinda mauti ndipo tutakapovikwa miili ya kutokufa na kuiluza mauti kuwapi kushinda kwako?? 1wakorintho 15:55 Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?... Tamanio langu ni kumuona Kristo ajapo mara ya pili, ikiwa ndio tamanio lako muombe Mungu leo akupatie ROHO MTAKATIFU akukumbushe kuzihesabu siku zako, uishi ukijiandaa muda wowote maana hatujui ni lini zamu yetu itafika.

BWANA AKUBARIKI

BY; PR. PETER I. JEFTER
0783167164
peterjefter91@gmail.com

No comments:

Post a Comment