Friday, 19 May 2017

MTU WA NNE KATIKATI YA MOTO



MTU WA NNE KATIKATI YA MOTO
(The forth man in the midst of fire)

Daniel 3:25 Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.

Bila shaka katika maisha ya kawaida imeozoeleka kuwa kila jamii huwa na desturi au tamaduni zake, na hivyo tamaduni hizo hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine. Kwa mfano tamaduni za kiafrika kwa sehemu kubwa hutofautiana na tamaduni za wazungu au waarabu wachina nk. Mambo haya ya kutofautiana kwa tamaduni hayakuanza leo lakini ni tangu miaka na miaka na hata katika habari za ibada pia kutofautiana kwa tamaduni kupo. Wakati wengine wakimwabudu Mungu wa kweli wengine wanaabudu Miungu mingine, wengine hutofautiana katika kubatiza wengine kufundisha biblia wengine hata siku za kuabudu.

Mpendwa msomaji naomba nikuulize swali, hebu fikiria katika tamaduni yako uliyoizoea labda iwe ni tamaduni ya kijamii au ya kiroho alafu ukaenda katika jamii nyingine ukakuta tamaduni nyingine tofauti kabisa na yako, hali ukijua ni mbaya na haifai kwako lakini sheria za jamii ile inakulazimisha kuacha tamaduni yako na kufuata ya kwao vinginevyo ukutane na adhabu kali amabyo huenda ni ya kifo, utafanyaje???????

Hali kama hii ndiyo inayowakuta vijana watatu wa kiebrania waliochukuliwa utumwani Babeli. Mara baada ya kufika Babeli vijana hawa walitakiwa kuacha kabisa desturi zao za kiebrania na kufuata desturi za wakaldayo (Babeli). Na hivyo jaribu la kwanza lilikuwa ni kuwabadilisha majina ili wawe na majina ya kibabeli Daniel 1:7 Mkuu wa matowashi akawapa majina; alimwita Danieli, Belteshaza; na Hanania akamwita Shadraka; na Mishaeli akamwita Meshaki; na Azaria akamwita Abednego. Kama hilo halikutosha walipaswa hata kula chakula cha wakaldayo Daniel 1:5 Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme. Lakini katika hili la chakula hawakuwa tayari kujitia unajisi kwayo hivyo waliazimu kutokula na zaidi wakapewa chakula kama kile walichozoea

Vijana hawa walionekana kuwa na maarifa na hekima zaidi sana walikuwa pia ni wazuri wa sura Daniel 1:4,6vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao. Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda, Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria. Na hio kwa sababu ya mafanikio haya wakaldayo hawakuwa na furaha juu yao wakakusudia kuwaangamiza. 

Na sasa walitakiwa kuacha tamaduni yao ya kumwabudu Mungu wao wa kweli na kuabudu Miungu ya wakaldayo. Katika tamadani ya wakaldayo waliabudu Miungu kama vile sanamu nk. Mfalme Nebukadneza anaamuru sanamu itengenezwe kubwa Daniel 3:1 Nebukadreza, mfalme, alifanya sanamu ya dhahabu, ambayo urefu wake ulikuwa ni dhiraa sitini, na upana wake dhiraa sita; akaisimamisha katika uwanda wa Dura, katika wilaya ya Babeli. Na akaamuru watu wote waletwe wasujudie sanamu ile. Ama lah! Atakayekataa kuisujudia sanamu ile atatupwa katika tanuru la moto mara moja.Daniel 3:6 Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao.

Kiashiria tu kiliposikika kila mtu alipaswa kuanguka na kusujudia sanamu ile Daniel 3:5 wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Katika hali isiyoweza kuelezeka hili lilikuwa ni jaribu kuu na kubwa kwa vijana waebrania ambao sasa wanalazimishwa kumuasi Mungu wao lakini ashukuriwe Mungu vijana hawa hawakuwa tayari kufanya hivyo. Ndipo kila aina ya ngoma iliposikika wakaldayo wote walianguka na kuisujudia sanamu ile isipokuwa wale vijana watatu tu wa kiebrania. Daniel 3:12 Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Vijana hawa walitambua ya kuwa kusujudu na kuabudu ni tendo la heshima kwa Mungu wa mbinguni pekee yake na hivyo kusujudia sanamu ilikuwa ni kuasi juu ya sheria ya Mungu mathayo 4:10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Soma pia (kutoka 20:4, 5)

Kutokana na kitendo hicho hakika ghadhabu ya mfalme ilipanda hata kuwauliza vijana kama huenda ni kwa makusudi walikataa kutii amri ya mfalme, ndipo mfalme Nebukadneza kwa ujinga wake akadhani kwa kuwapa nafasi ya pili wangethubutu hata kuinamisha vichwa Daniel 3:15 Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu? Vijana hawa kwa kutambua ukuu wa Mungu kwao hawakuwa na sababu ya kusujudia sanamu ya mfalme walichomwambia mfalme ni Daniel 3:16-18Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Bila shaka vijana hawakuona haja ya kusujudia sanamu ile.

Kwa sababu hasira ya mfalme ilikuwa kali sana juu ya vijana wale aliamuru moto uongezwe mara saba na kuamuru vijana wale watupwe ndni ya lile tanuru la moto hali wamefungwa Daniel 3:19, 20 Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Na kwa sababu ya ukali wa moto huu waliokufa wa kwanza walikuwa ni wanajeshi wa Nebukadneza waliomuriwa kuwatupa vijana wale ndani ya moto.

AJABU KULIKO AJABU ZOTE DUNIANI, Vijana hawa walitupwa ndani ya tanuru wakiwa watatu hali wamefungwa lakini sasa mfalme anaona wakiwa wanne hali wamefunguliwa na hawajadhurika hata kidogo. Tendo hili lilimtoa mfalme akili kidogo hata kushindwa kuelewa kama ni ya kweli anayoyaona au huenda anaota ikabidi atafute ushahidi kwa waliokuwa karibu naye huenda nao walikuwa wanaona. Lakini ndivyo ilivyokuwa wala Daniel 3:24, 25 Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Jambo linalomshangaza mfalme ni kuwa walitupwa watatu na sasa anawaona wanne tena yule wanne ana sura ya mwana wa Mungu. Kumbe hata mfalme alimtambua mwana wa Mungu JINA LA BWANA LITUKUZWE.

Ndipo mfalme akaamuru vijana wale watolewe ndani ya tanuru na kutoa agizo kwa kila mtu kumuabudu Mungu wa shadrack Meshack Shadrack na Abednego Daniel 3:28 Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe.kisha mfalme akawatukuza vijana wale (fungu la 30)

Mpendwa rafiki je umeogopa kwa ajili ya moto uliowashwa kwa ajili yako??? Nakukumbusha kuwa yupo mtu wanne ataonekana katika tanuru la moto lililowashwa kwa ajili yako. Yohana 16:33 Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu. Huenda ni kwa sababu ya mafanikio yako moto utawashwa kwa ajili yako ili ushushwe, huenda ni kwa sababu ya mali, utajiri, uwezo, au hata uzuri majaribu yatakuijia yenye ukali kama wa moto wa Nebukadneza usiogope maana mtu wanne ataonekana. Huenda ni kwa sababu ya imani yako matahayo 10:17-19 Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema.

hata sasa jaribu la kuabudu sanamu ya mnyama iko mbele yetu nalo litatolewa tangazo kama lile la mfalme Nebukadneza. Ufunuo 13:15 Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe. Haya yote yajapotupata hatuna haja ya kuogopa kwa maana mtu wanne yupo nasi tukawe na jibu kama lile la kina shadrack, Meshack na Abednego Daniel 3:16-18Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
NAWATAKIENI BARAKA ZA BWANA

WENU MJOLI WA BABA
PETER I.JEFTER
0783167164
peterjefter91@gmail.com/pierredejr2000@gmail.com

5 comments:

  1. Im blessed...songa mbele kwa neema ya Bwana

    ReplyDelete
  2. Mungu akubariki kwa hubiri hili. Nimebarikiwa sana

    ReplyDelete
  3. Baada ya hawa vijana kutoka katika tanuru walipotelea wapi?Hatuwaoni teni!

    ReplyDelete
  4. Je vijana hawa walikua na familia?

    ReplyDelete