Friday, 19 May 2017

SIMAMA TAZAMA KALVARI

SIMAMA TAZAMA KALVARI

1Wakorintho 1:18 Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.

Matokeo ya dhambi yalipelekea kusudi zima la Mungu kuumba dunia kutoweka. Hapo awali Mungu aliumba dunia katika uzuri na ukamilifu wake na kila alichofanya Mungu kilikuwa ni chema Mwanzo 1:31 Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita. Na hivyo mpango wa Mungu ulikuwa ni kufanya kila kitu kiwe chema na duniani pawe mahali pema kwa binadamu na viumbe vingine vyote alivyoviumba Mungu.

Mara tu baada ya anguko la mwanadamu dhambini kila kitu kilibadilika na uso wa dunia uligubikwa na huzuni kwa kuwa muasi ameleta badiliko hasi tofauti na kile Mungu alichokusudia. Dunia iliyoumbwa na Mungu kila kitu kikawa ni chema sasa kinabadilika na kuwa dunia iliyolaaniwa Mwanzo 3;17……. Ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako,uadui na chuki vikaingia katika ulimwengu, viumbe vilivyoumbwa katika ukamilifu vikabadilika na kuiona matokeo ya aanguko ikiwapelekea laana. Dunia nzima ikapoteza maana yake dhambi ikaingia duniani na kwa kuanguka kwake mtu mmoja ulimwengu wote ukahesabiwa adhabu ya kifo. warumi 5:18,19 Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima.Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.

Matokeo ya Shetani kuasi mbinguni yameipelekea dunia kuwa si tena mahali panapotamanika, dunia imepoteza kabisa maana yake, dunia imekuwa tena si mahali ambapo bado watu wanatamani kukaa dunia imepoteza tumaini. Matukio makubwa na ya kutisha yameuteka ulimwengu, ajali, vifo, vita, njaa, matetemeko ya ardhi, uasi dhidi ya sheria ya Mungu, chuki kati ya ndugu, jamaa, marafiki, wenzi, nk nk. Dunia haitamaniki tena wapendwa. 

Maisha ya mwanadamu yamegubikwa na dhambi kila siku, huzuni, majonzi, misiba, vilio njaa na shida za kila namna. Watu hawajui wafanye nini, hawajui waende wapi hawajui wakimbilie wapi, watu hawaoni tena faraja kutoka kwa ndugu zao jamaa zao hata watu wao wa karibu nao ndio wamekuwa ni wasaliti kwao kila siku. Dunia imekuwa si tena mahali salama kwao

JE UNAFANYA NINI UNAPOJIKUTA MWENYEWE??
Pamoja na dunia kulaaniwa na dhumuni lake kubadilika kabisa kutoka katika ule mpango wa awali wa Mungu lakini bado Mungu hakumwacha mwanadamu awe pekee yake. Hata pale Adam na Hawa walipoanguka kwa kula tunda bado neema ya Mungu ilikuwa juu yao naye Mungu alilazimika kutoa kafara ya mwanakondoo ili iwe kipatanisho kati ya mwanadamu mdhambi na Mungu muumbaji, bado ngozi yake ilitumika kuficha aibu ya uchi wa mwanadamu aliyekimbia kujificha pia akaweka uadui kati ya mwanadmu na nyoka (shetani) mwanzo 3:15 nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.

Upendo wa Mungu alio mwingi kwa wanadamu wote bado ulikuwa juu ya mwanadamu mdhambi, na kwa sababu hiyo bado akaona haitoshi kuthibitisha upendo huo hata kumtoa mwanawe pekee ili kuleta ukombozi kwa dunia yote iliyoanguka. Yohana 3:16 wa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Ni kwa sababu ya upendo mwingi wa Mungu hata alidiriki kumtuma mwanawe pekee Yesu Kristo kuja kufa msalabani ili kuleta ondoleo la dhambi, ili kuleta faraja kwao wenye huzuni, ili kuleta tumaini kwao wapotezao tumaini, ili kuleta ukombozi kwao wapoteao, ili kuleta amani kwao wachukianao ili kuleta furaha kwao wahuzunikao.

Kwa upendo huo ilimlazimu Mwana wa Mungu kupitia kifo cha aibu, kifo cha laana, kifo cha dharau kifo cha ukatili ili sisi tupate ondoleo la dhambi na ukombozi kwa ajili ya maisha yetu. Alikubali kuchukua dhambi zetu na kujitwika, alikubali kudharauliwa kwa ajili yetu, alikubali kuudhiwa kwa ajili ya ukombozi wetu alikubali kubeba aibu yetu na adhabu ya amani yetu iliwekwa juu yake Isaya 53:3,4 Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.

Ni kupitia kifo cha msalaba ndipo Kristo alipoleta ondoleo la dhambi kwao wamwaminio. Ilimpasa kupitia kifo cha msalaba ili kupatanisha ulimwengu na mbingu, kumpatanisha mwanadamu mdhambi na Mungu mkamilifu. Wakolosai 1:20 kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.


SIMAMA TAZAMA KALVARI
Ni kupitia kalvari Kristo alitupatanisha na Mungu, “uniangalie atwambia, Yesu aliye tufia msalabani ni uzima, hapa utaipata uzima.. kutazama kalwari, kutazama kalwari ni kupewa kuishi kutazama mti”.. hata ijapo tunapitia magumu kiasi gani, hata ijapo dunia imepotea kiasi gani, hata ijapo dunia imepoteza tumaini bado tumaini letu lipo kwake Kristo. Ni kwa kutazama msalaba twapata tumaini, ni kwa kutazama msalaba twapata ondoleo la dhambi, ni kwa kutazama msalaba twapata faraja, kupitia msalaba twapata amani, kupitia msalaba twapata wokovu wa maisha yetu maana ni kupitia msalaba Kristo alifanyika kafara ya milele. Wakolosai 2:14,15akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.

Usikatishwe tamaa wala usizuiliwe na jambo lolote, tumaini lako liweke kwa Kristo pekee. Simama tazama kalvari ukutane na Kristo yeye aliyeichukua aibu yetu, yeye alikubali kudharauliwa kwa ajili ya wokovu wangu na wako waebrania 12:2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

Ni kuptia msalaba hao wamwaminio wataokolewa lakini kwao wapoteao ni upuuzi…….. 1Wakorintho 1:18 Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.

BWANA AWABARIKI

By Pierre de' Jefter
0783167164
pierredejr2000@gmail.com

No comments:

Post a Comment