Friday, 19 May 2017

TUMAINI KATIKATI YA MAOMBOLEZO



TUMAINI KATIKATI YA MAOMBOLEZO


Yeremia 29:11 Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.

Kijana mmoja (John) anasimulia hivi; ilikuwa ni mwaka 2008 march ndiyo uliyokuwa mwisho wake kumuona Baba yake mzazi, akiwa ameishi na Baba yake kwa takribani miaka 17 ghafla siku moja akiwa shule alipokea taarifa za msiba wa Baba yake mzazi. Kijana huyu anasema aliposikia habari zile alishindwa kuamini kama ni kweli au si kweli. Ilimchukua zaidi ya nusu saa kurudia hali yake ya kawaida ili kuendelea kutafuta ukweli wa jambo lile. Lakini ilikuwa ni kweli mzazi wa kijana huyu alikuwa amefariki siku ile.

Kutokana na taarifa zile kijana huyu aliona kama naye muda wake wa kuishi duniani umefikia ukomo, kwani hakuona tena tumaini mbeleni kwa sababu mzazi wake huyu ndiye aliyekuwa kila kitu kwake kwani mama yake alishafariki miaka minne nyuma (2004), John alijua amepoteza kila kitu na hata elimu yake aliyokuwa akitafuta ilikuwa imefika mwisho. Mnamo siku ya mazishi ya Baba yake kijana John alipoteza fahamu kutokana na kilio kilichojaa uchungu kwa kuwa alipoteza tumaini ya siku za usoni. Mara ghafla sauti ya shangazi yake ilisikika masikioni mwake ikimbembeleza na kumsihi anyamae (nyamaza John usilie sana, nyamaza tu kama ni shule bado utaendelea na usihofu sana tutakusaidia, sauti ya shangazi). Hii ndiyo iliyokuwa sauti iliyoleta tumaini kwa kijana peter kwakuwa aliona yupo mfariji kwake ……………

Sura ya 29 ya kitabu cha Yeremia ni barua ambayo MUNGU anamuongoza yeremia kuandika na kuituma kwa watu walio uhamishoni (Babeli) ukiwa umejaa ujumbe wa matumaini. Yeremia 29:1 Maneno haya ndiyo maneno ya waraka, ambao nabii Yeremia aliupeleka toka Yerusalemu, kwa hao waliobaki wa wakuu waliochukuliwa mateka, na kwa makuhani, na kwa manabii, na kwa watu wote, ambao Nebukadreza aliwachukua mateka toka Yerusalemu hata Babeli; ieleweke kuwa wakati wana wa Israeli wakichukuliwa utumwani Yeremia alibaki Yerusalemu

Wana wa Israeli kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao na uasi wao na viongozi wao dhidi ya sheria ya Mungu, Mungu aliamuru watiwe mikononi mwa wafalme wa mataifa walioitawala dunia kwa wakati huo (Nebuchadnezzar mfalme wa Babeli) Yeremia 25:8,9 Basi Bwana wa majeshi asema hivi, Kwa kuwa hamkuyasikiliza maneno yangu, angalieni, nitapeleka watu na kuzitwaa jamaa zote za upande wa kaskazini, asema Bwana, nami nitatuma ujumbe kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu, nami nitawaleta juu ya nchi hii, na juu yao wakaao ndani yake, na juu ya mataifa haya yote yaliyopo pande zote; nami nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kitu cha kushangaza, na kitu cha kuzomewa, na ukiwa wa daima.

Na hivyo iliwapasa kukaa utumwani kwa miaka 70. Yeremia 25:12 Na itakuwa miaka hiyo sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na taifa lile, asema Bwana, kwa sababu ya uovu wao, nayo nchi ya Wakaldayo pia; nami nitaifanya kuwa ukiwa wa milele. Ujumbe wa sura ya 29 unapotumwa ndipo tu miaka 10 ilikuwa imepita kwahiyo vijana bado walikuwa na safari ya miaka 60 kuendelea kukaa utumwani (kwa msaada kwako msomaji wana wa Israeli walipelekwa Babeli kwa mara ya kwanza mwaka 605 K.K na ilipofika mwaka 539 K.K ndipo ulipofika mwisho wake). 

Katika kipindi hiki kigumu ambacho watu hawa wa Mungu waliomuasi wanapitia nyakati ngumu za utumwa (fikiria hali ya kufanywa kuwa mtumwa katika nchi ya ugeni, taifa lililokuwa likiongozwa na kiongozi dictator na katili ajabu Nebukadneza), bila shaka wana wa Israeli walipoteza matumaini kabisa na huenda hawakuona tena ukombozi mbele yao hasa katika taifa la kijeshi lililotawala dunia nzima.

Makosa yaliyofanywa na viongozi na wana wa Israeli yalikuwa ni kukataa maonyo ya Mungu yaliyoletwa kwao kupitia kwa watumishi wa Mungu, kumbuka hata safari ya Israeli kutoka Misri kwenda Kaanan mioyo yao ilikuwa migumu hakika. Katika kipindi hiki Mungu anamtumia nabii wake Yeremia kupeleka maonyo kwa viongozi na raia lakini hakuna hata aliyeonekana kujali. Si kiongozi wala si mwananchi aliyeonekana kusikiza kile Mungu alichonena kupitia kwa nabii Yeremia 

Pamoja na uasi mkuu wa namna hiyo, pamoja na kukaa utumwani kwa muda wote huo lakini bado BWANA hakuwasahau watu hawa. UPENDO MKUU ULIOJE!! . ujumbe wa matumaini unatumwa kwa watu waliopoteza tumaini. Bila shaka watu hawa walikuwa katika hali ya masikitiko na maombolezo mengi kwa sababu ya mateso, dhiki na manyanyaso mengi waliyokuwa wakiyapitia katika nchi ya ugeni. Huenda hawakujua ni wapi wokovu wao ungepatikana hasa ukiangalia aliyekuwa kiongozi wao kwa wakati huo (Yehoyakini) alifanywa mateka pamoja na familia yake na walielewa wazi ya kuwa huenda Mungu asingewaletea

ukombozi tena kwa kuwa walishayaacha maagizo yake na hivyo walijua hakika Mungu amewaacha.
Habari pekee inayoleta matumaini kwa watumwa hawa (wana wa Israeli) inatoka kwa yule yule aliyeruhusu waende utumwani, naye ni Mungu pekee. Hili hutufundisha upendo mkuu wa ajabu na usioelezeka alionao Mungu kwa watu wake hata wajapomuasi kwa kiasi gani.Yeremia 29:10 Maana Bwana asema hivi, Babeli utakapotimiziwa miaka sabini, nitawajilia ninyi, na kulitimiza neno langu jema kwenu, kwa kuwarudisha mahali hapa. Mungu alitaka wana wa Israeli watambue ukuu wake lakini bado mioyo yao ilikuwa migumu. Bwana akaamua kuwaadhibu kupitia kwa utawala wa kidunia. Hivyo iliwapasa kukaa utumwani kwa muda wa miaka 70 ndipo wokovu utakapowajia.

Ndipo Mungu huyu huyu waliyemkataa na kumuasi anawapa ujumbe uliojaa tumaini ujumbe unaoleta faraja katika nyakati za za maombolezo na huzuni nyingi. Yeremia 29:11 Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Hii ilikuwa ni habari njema kwa watumwa hawa waliomkataa Bwana wao. Kumbe siku zote za matukio makubwa kama hayo bado Bwana aliwawazia mawazo ya amani wala si ya mabaya lakini zaidi sana kuwapa tumaini katika siku za mwisho. Mipango ya Mungu juu ya wokovu wa wana wa Israeli toka utumwani bado ulikuwepo lakini safari hii ilikuwa ni mpaka zitimie miaka 70.

Pamoja na maovu yote ambayo wana wa Israeli walitenda, pamoja na uasi wote ambao wana wa Israeli walifanya dhidi ya maonyo ya Bwana lakini bado Rehema za Bwana zilikuwa juu yao, neema na upendo mwingi wa Bwana bado ulikuwa pamoja nao. Na hivyo iliwapasa wana wa Israel kumtafuta Bwana na kumrudia Yeremia 29:12-14 Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. Nami nitaonekana kwenu, asema Bwana, nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema Bwana; nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka. Iliwapasa wana wa Israeli kuutafuta uso wa Mungu hata katika nyakati ngumu za namna gani walizokuwa wakipitia.

Wengi wetu leo tupo katika utumwa mzito tena mgumu wa dhambi, haya yote ni matokeo ya kukataa kusikia na kutii sauti ya Mungu. Kama ilivyokuwa katika siku za wana wa Israeli. Mungu ameruhusu tupitie katika vifungo hivyo vya utumwa kwa sababu ya kukataa kutii maagizo yake leo. Mathayo 15:8, 9 Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.

Kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli ndivyo ambavyo imekuwa hata leo. Sauti ya Mungu tumeisikia lakini hatujataka kuenenda kama inavyotuagiza. Wengu wetu tupo katika utumwa wa dhambi, dhambi za uongo, ulevi, uasherati, wizi, masengenyo, kuabudu sanamu, uzinzi na kila aina ya dhambi wengine wanapitia hali ngumu za maisha njaa, magonjwa, misiba nk. Pamoja na hayo yote bado ujumbe ule ule wa matumaini uliotoka kwa Mungu kwenda kwa wana wa Israeli waliokuwa utumwani ujumbe wa amani na matumaini bado unakuja kwetu hata leo. Bwana hajatuacha kwa sababu ya hali zetu za dhambi, Bwana hajatuacha wapendwa kwa sababu ya kutanga mbali naye bado anatuita leo tumrudie naye atatufanya kuwa wapya. Huenda miaka yako 70 ya utumwa wa dhambi ya uzinzi ni leo, huenda huu ndio muda wako wa kuokolewa. Mathayo 11:28, 29 Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; huu ndio wito wa Bwana kwetu leo, yeye Mungu anayetuwazia mawazo ya amani anatuita twende tusemezane 

Isaya 1:18, 19 Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; Upendo, neema na Rehema za Mungu bado zipo nasi hata leo imetupasa kumtafuta Bwana maadam anapatikana. Isaya 55:6,7 Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.

Rehema za Mungu zipo kwa kila amtafutaye, tazama saa ya wakovu kwako ndiyo sasa saa iliyokubalika ndiyo hii. 2wakorintho 6:2 Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa) Mrudie Bwana maana yupo tayari anakungoja. (Ufunuo 3:20, 21)

BWANA AWABARIKI.

Peter Jefter
0783167164
pierredejr2000@gmail.com





No comments:

Post a Comment