Sunday, 21 May 2017

KILIO CHA USIKU WA MANANE



                                           KILIO CHA USIKU WA MANANE
                                                     (MIDNIGHT CRY)

Mathayo 25:6 Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.

Bila shaka tukizungumzia arusi hakuna yeyote anayeweza kuwa na swali juu ya namna arusi inavokuwa. Katika arusi kwa kawaida lazima kuwepo na Bwana arusi, Bibi harusi, wapambe vyakula nk. Kwahiyo sherehe inakuwa kubwa watu wanafurahi siku hiyo na hasa kwa anayeoa au anayeolewa na hata ndugu jamaa na marafiki. Kwa kweli furaha ya arusi ni ya pekee ambayo kila mtu maishani mwake hubaki kusimulia popote anapokuwepo.

Katika mafundisho ya Yesu kwa wanafunzi wake na hata makutano waliomzunguka alipenda sana kufundisha juu ya ufalme wa Mbinguni (ufalme wa Mungu kama inavyoweza kuzoeleka kwa wengine) na ndiyo maana aliwapa pia wanafunzi wake jukumu la kuhubiri juu yua ufalme wa Mbinguni. Mathayo 10: 7 Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.

Katika sura ya 25:1-13 ya kitabu cha mathayo Yesu anatumia kisa cha Arusi kutoa fundisho muhimu juu ya ufalme wa mbinguni na maandalizi ya wale wanaohusika katika arusi hiyo. Mathayo 25:1-5 Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. 2 Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. 3 Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; 4 bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. 5 Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi

Kisa hiki Yesu anakitoa maalum sio kutujengea mazingira ya kuelewa arusi inavyokuwa lakini kutupatia picha halisi juu ya ufalme wa mbinguni na marejeo yake kuwafuata walio wake. Katika kisa hiki kuna wanawali kumi wakiwa katika makundi mawili tofauti watano wakiwa ni wapumbavu na watano wakiwa wenye busara. Wengine waweza kudhani kuwa kisa hiki huzungumzia makundi mawili ya walio kanisani na walio nje ya kanisa LA!

Somo hili huzungumza juu ya watu wote waliomo ndani ya kanisa na halina uhusiano kabisa na walio nje ya kanisa kama ambavyo wengine wanaweza kudhani. Sababu zifuatazo huthibitisha kuwa wanawali hawa huwakilisha watu waliomo ndani ya kanisa. 1, wote ni wanawali maana kuwa wote wamejiandaa na tukio la Arusi (kurejea kwa mwokozi), 2. Wote wana taa lakini ni wenye busara tu ndio waliohifadhi mafuta wapumbavu hawakukumbuka kuhifadhi mafuta maana yake ni kuwa wote walipokea nuru lakini ni wachache walikubali kuitumia ile nuru waliopokea.

Kwa kufafanua zaidi makundi haya mawili tuanze kwa kuangalia kundi la wapumbavu. Kama ambavyo tumekwisha kuona kuwa wanawakilisha watu waliomo ndani ya kanisa waliopokea kweli ya Biblia lakini hawakuwa tayari kubadilishwa na ile kweli, maandalizi yao ya kumpokea bwana arusi (Yesu kristo) haukufanyika katika viwango vinavyopaswa. Pamoja na kuisikia sauti ya Mungu kila siku lakini hawakukubali kubadilisha maisha yao na kumfuata. Kila siku walisikia maonyo juu ya maovu yao lakini hawakuwa tayari kuacha, walisikia miito juu ya kufanya matengenezo katika maisha hayo lakini hawakujali. Walienda kanisani kama desturi lakini hawakuelewa maana halisi ya kwenda kanisani, na wakidai kujiandaa na marejeo ya pili ya Yesu kristo Ezekiel 33: 31 Nao huja kwako kama watu wajavyo, nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao husikia maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo mwingi, lakini mioyo yao inatafuta faida yao. Soma pia mathayo 15:8

Kundi hili pia huonesha kuishiwa mafuta ya taa wakati wa kuwasili kwa Bwana arusi wakati wa siku wa manane humaanisha kuelemewa na maisha ya ulimwengu na yaliyomo hata kujisahau kuwa tayari kwa marejeo ya mwakozi. Wanawali wapumbavu walikuwa na mafuta kidogo kiasi cha kwamba isingeweza kustahimili hata wakati wa usiku wa manane anapokuja bwana arusi, maana yake ni kwamba wale walio ndani ya kanisa na wanauelewa mdogo wa kweli hataweza kustahimili dhoruba zitazowapata wale wanaomngojea kristo. Lakini pia hawa wanawali wapumbavu wanaonekana walitarajia marejeo ya bwana arusi kutokea mapema hali amechelewa hadi usiku wa manane, ndivyo ilvyo kwao hao walio ndani ya kanisa wakitarajia marejeo ya Yesu kuja upesi na wanapoona kristo anachelewa hulala usingizi wa kiroho na kujisahau kabisa kufanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kumpokea Kristo, hawa ndio wale walioingia harusini bila vazimaalum la arusi 

Kundi la pili katika kisa hiki ni kundi la wanawali watano wenye busara waliotunza mafuta yao hata alipokuja bwana arusi. Kundi hili huwakilisha kundi la wafuasi halisi wa kristo wale wanamatengenezo safi walioisikia sauti ya Mungu na kuruhusu mabadiliko ya kweli katika mioyo yao. 

Hawa ni wale ambao walipoisikia sauti ya Mungu hawakugeuza miguu yao kuzirudia njia zao mbaya za zamani. Mathayo 2: 12 Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Kutunza mafuta hata wakati wa usiku ni maandalizi mazuri ya kungojea marejeo ya pili ya mwokozi bila kujali ni lini atakuja. Hili ni kundi la wale waliompokea roho na kukubali kuongozwa nayo. Yohana 14:16,17 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.

Mara ilipofika usiku wa manane ndipo kelele ziliposikika mathayo 25:6 Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. (And at midnight there was a cry made, Behold, the bridegroom cometh; go ye out to meet him .KJV). Biblia ya kingereza (toleo la king james) huzungumzia kile kinachozungumzwa katika biblia ya Kiswahili kama kelele kuwa ni kilio (cry), ambayo humaanisha kuwa wakati alipowasili Bwana arusi katika mji kulitokea kilio. Huenda watu hawa walilia kwa sababu hawakutarajia ujio wa Bwana arusi katika nyakati zile, yawezekana walishajisemea moyoni kuwa Bwana arusi amechelewa au ameghairi safari. ya arusi na hivyo watu wakalala. Ni hivyo kutokea kwa Bwana arusi katika wakati ule ulisababisha mshtukizo mkubwa kwa walio wengi.

Ndipo wanawali wote wakashtuka kwenda kumlaki Bwana arusi mathayo 25:7 Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao habari mbaya zaidi ni kwamba waliposhtuka wale wapumbavu walijikuta taa zao zikishindwa kuwaka. Kwa haraka njia walioona sahihi kwao ni kuomba mafuta hata kidogo kwa wale wenye hekima ili angalau taa zao zistahimili mikiki ya usiku ule. 

Kile kinachozungumzwa katika Biblia kama usiku wa manane ajapo bwana arusi humaanisha giza la kiroho, giza la kiroho lipo karibu kuifunika dunia kwa kuwa watu wameikataa kweli Amosi 8:11,12 Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana. Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione. kutokuwepo kwa nuru tena kwa walio wengi. Watu watalala usingizi wa kiroho kwa kudhani kuwa mwokozi amechelewa kuja watu watajisahaulisha kuendelea kutafuta ukweli wa biblia. Kama ilivyokuwa katika kipindi cha nuhu ndivyo itakavyokuwa kipindi hiki ajapo mwokozi wa ulimwengu. luka 17:26, 27 Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Kama ilivyokuwa katika siku ya gharika watu walipomkimbilia nuhu wakihitaji wafunguliwe waingie kuepuka kifo cha milele lakini Nuhu hakuwa na uwezo wa kufungua safina ndivyo walivyokimbia wanawali wapumbavu wakihitaji msaada wa mafuta na wo wanawali wenye hekima hawakuweza kuwapatia mafuta, ndivyo itakavyokuwa kwetu pia, vile tutapuuzia kujiandaa kwa ajili ya siku ya ujio wa Bwana hatutaweza kupata msaada wowote toka kwa mtu yeyote yule. Ni fundisho kwetu kuwa maandalizi ya mtu mwingine hayataweza kumwokoa mtu mwingine na imani ya mtu haiwezi kuokoa imani ya mwingine, hivyo imetupasa kujiandaa maadam kungali bado mchana

Wakati ambapo watu watakuwa wamejisahau kuutafuta ukweli wa Mungu, wakati ambapo ulimwengu utakuwa umekuwa busy kwa shughuli za maendeleo, wakati wakazi wa ulimwengu wakifurahisha kwa anasa na kila aina ya starehe za kidunia ndipo atakapokuja mwana wa adamu. 1 wathesalonike 5:3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. Hakuna binadamu awaye yote atakayeweza kuokolewa kwa maandalizi hafifu. Yatupasa kujiandaa kungali mapema na tujiweke tayari kwa ujio wa mwokozi.

Matahyo 24:42-44 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja. Ni fundisho kwetu kuwa tusikadirie muda wa marejeo ya mwokozi na hapo tuonapo kuchelewa tunakata tama, imetupasa kujiandaa kila iitwapo leo kumlaki mwokozi maana saa yaja hatoweza mtu kufanya maandalizi yoyote. Imetupasa kukesha kwa maombi. 1 wathesalonike 5:17 ombeni bila kukoma. Kwa maana hatuijui siku wala saa atakapokuja. Na atakapokuja tusijekuwa kama wale wanawali wapumbavu

BWANA AWABARIKI

BY; PETER I. JEFTER
0783167164
peterjefter91@gmail.com

No comments:

Post a Comment